28 Mei 2026 - 14:36
Israel Yakiri Kushindwa Kukabiliana na Droni za Muqawama wa Lebanon

Jeshi la Israel limekiri kuwepo kwa hitilafu katika mifumo yake ya onyo dhidi ya droni za FPV zinazotumiwa na Muqawama wa Hezbollah, huku ripoti zikieleza kuwa teknolojia mpya ya droni hizo zinazoongozwa kwa “fiber-optic” imeongeza hofu na changamoto kubwa kwa vikosi vya utawala huo katika medani za mapambano.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa jeshi la utawala huo linakabiliwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na droni za mashambulizi za FPV zinazotumiwa na makundi ya Muqawama.

Televisheni ya Channel 12 ya Israel imesema jeshi hilo limekiri kuwepo kwa hitilafu katika mfumo wake wa kutoa onyo mapema dhidi ya droni hizo, jambo lililoibua hofu mpya kuhusu uwezo wake wa kiulinzi katika maeneo ya mapambano.

Wakati huohuo, gazeti la Haaretz limeripoti kuwa viongozi wa kijeshi wa Israel wana wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la matumizi ya droni zilizobeba vilipuzi, huku wakikiri wazi kuwa hawana mfumo madhubuti wa kuzikabili kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi kilichonukuliwa na gazeti hilo, jeshi la Israel “halikuwa limejiandaa” kwa aina hii ya mashambulizi, jambo ambalo limeongeza shinikizo kwa makamanda wa kijeshi, wanajeshi waliopo mstari wa mbele pamoja na familia zao.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa operesheni za ardhini zilizopanuliwa katika maeneo ya kaskazini, zilizolenga kuzuia urushwaji wa droni kuelekea makazi ya walowezi, bado hazijafanikiwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, kusonga mbele kwa vikosi vya Israel katika maeneo ya mapambano kumeendelea kuwaweka wanajeshi wake katika hatari zaidi, huku wakilengwa kwa urahisi na droni zinazoongozwa kupitia mfumo wa mawasiliano wa “fiber-optic”, ambazo zinaelezwa kuwa ni ngumu kuzizuia kwa njia za kawaida za kimawasiliano au kuzidungua angani.

Ripoti hizo zinaashiria kuongezeka kwa changamoto za kiusalama kwa jeshi la Israel, hasa katika kukabiliana na teknolojia mpya zinazotumiwa na makundi ya Muqawama katika medani za mapambano.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha